Entertainment

Willy Paul akosolewa kwa kutumia Kshs millioni 3.5 kuandaa video ya wimbo wake

Willy Paul akosolewa kwa kutumia Kshs millioni 3.5 kuandaa video ya wimbo wake

Staa wa muziki nchini Kenya Willy Paul anazidi kupata ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki mbali mbali wa muziki baada ya msanii huyo kuweka wazi kuwa alitumia kiasi cha shillingi millioni 3.5 kuandaa video ya wimbo wake mpya ‘Keki’ aliyomshirikisha Bahati.

Kupitia post aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram akijinadi kutumia kiasi hicho cha fedha kwenye uandaaji wa video ya ngoma hiyo, baadhi ya mashabiki walioachia maoni yao kwenye chapisho hilo wameonekana kutofurahia viwango alivyoonesha kwenye nyimbo alizoziachia rasmi Januari 31 ambazo ni Keki pamoja na Paah.

Kulingana na kauli za mashabiki, licha ya Willy Paul kutumia nguvu nyingi kutangaza ujio wa kazi hizo, alifeli kwenye suala la uandishi wa nyimbo wakihoji kuwa msanii ameishiwa na ubunifu wa kutoa nyimbo za kuvutia. Aidha wamempa changamoto kuwatafuta waandishi wazuri wa nyimbo na kuwalipa ili waweze kumuandikia nyimbo ambazo zina maudhui ya kuburudisha jamii sambamba na kuelimisha.

Katika hatua nyingine wamemshauri kubadilisha prodyuza anayetayarisha kazi zake za muziki kutokana na kukosa ubunifu wa kuandaa nyimbo zinazoendana na nyakati zilizopo.

Willy Paul ambaye yupo mbioni kuandaa tamasha lake muziki mnamo Februari 14 mwaka huu amepokea ukosoaji mkubwa sio tu kutoka kwa mashabiki bali pia kutoka kwa maprodyuza wa muziki nchini, wa hivi punde akiwa ni prodyuza Vinc on The Beat ambaye ameonekana kutoridhishwa na kiwango cha msanii huyo baada ya kuachia nyimbo mbili kwa pamoja alizomshirikisha msanii Bahati ambaye ni hasimu wake wa muda mrefu kwenye muziki.