
Msanii wa muziki wa rap nchini Kenya, Wangechi, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kuandika ujumbe wa kutatanisha unaoashiria kuwepo kwa unyonyaji na hujuma dhidi ya wasanii wa kike katika tasnia ya muziki humu nchini.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Wangechi alidokeza kuwa kuna mtu mashuhuri kwenye sekta ya muziki humu nchini anayefanana na mtayarishaji wa muziki wa Marekani, Diddy ambaye kwa miaka amezuia wasanii wa kike kutoka na kazi zao kutoka studio.
“One day we shall speak about the Diddy of Kenya and how no female artist ever left that studio with their music.”
(“Siku moja tutazungumza kuhusu Diddy wa Kenya na jinsi hakuna msanii wa kike aliyewahi kutoka katika studio hiyo na muziki wake.”) – aliandika Wangechi.
Ingawa hakumtaja mtu yeyote kwa jina, kauli hiyo imeibua mijadala mikubwa kuhusu usalama, haki na usawa katika sekta ya muziki hasa kwa wasanii wa kike ambao kwa muda mrefu wamelalamikia ukosefu wa usaidizi wa haki na kuwepo kwa mazingira yenye unyanyasaji wa kiakili, kijinsia na kitaaluma.
Mashabiki na wadau wa muziki wameanza kujiuliza ni nani “Diddy wa Kenya” anayetajwa, huku wengi wakihusisha ujumbe huo na visa vya awali vilivyoripotiwa na baadhi ya wanamuziki wachanga.
Hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, Wangechi bado hajatoa maelezo zaidi, lakini ujumbe wake umeacha gumzo zito ambalo huenda likabadilisha mwelekeo wa mazungumzo kuhusu usalama, uhuru na haki za wasanii wa kike nchini Kenya.