
Mahakama Kuu ya Milimani imeamua kwamba Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Kenya – KFCB haina mamlaka ya kulazimisha watayarishaji wa maudhui ya kawaida mitandaoni kulipa ada za leseni chini ya sheria ya sasa ya filamu.
Uamuzi huo umetolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwanamuziki William Getumbe Kinyanjui, aliyepinga hatua ya KFCB ya kumtaka alipe shilingi elfu mia mbili arobaini na tatu na mia mbili (KSh 243,200) kwa video zake mbili alizopakia kwenye mtandao wa YouTube mapema mwaka huu. Video hizo, “Yesu Ninyandue – Imejaa” na “Yesu Ninyandue – Nyonga”, zilidaiwa na KFCB kuwa zisizofaa kwa umma, na taasisi hiyo ilimtaka aziondoe mara moja.
Getumbe alieleza kuwa video hizo, zilizorekodiwa kwa simu, hazikuhitaji leseni kwa kuwa hazikuwa filamu za kibiashara. Alidai kuwa hatua ya KFCB ilikiuka haki zake za kikatiba, zikiwemo uhuru wa kujieleza na haki ya kusikilizwa.
Katika uamuzi wake, mahakama ilisema kuwa sheria ya sasa ya filamu (Cap 222) haielekezi kuhusu video za kawaida mitandaoni, na hivyo haiwezi kutumika kumlazimisha mtu kulipa ada kwa video za simu zinazopakiwa kwenye mitandao kama YouTube, TikTok au Facebook. Mahakama pia ilitaja kuwa barua ya KFCB ya tarehe 29 Februari pamoja na ankara ya malipo ni batili na haina msingi wa kisheria.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Getumbe alionekana mwenye furaha na faraja, akisema:
“Nimeshukuru sana kwa haki kutendeka. Sauti yangu sasa imesikika. Kama msanii wa kawaida niliyekuwa nikipambana, nilihisi kunyanyaswa na kukandamizwa, lakini sasa najua kwamba hata sisi wa mitaani tuna haki sawa.”
Aliongeza kuwa uamuzi huo ni ushindi si kwake binafsi tu, bali kwa watayarishaji wote wa maudhui wanaotumia mitandao kama jukwaa la kujieleza.
Uamuzi huu unatarajiwa kuwa wa kihistoria, huku ukilenga kulinda uhuru wa maudhui mtandaoni na kuchochea mjadala wa kitaifa kuhusu namna bora ya kusimamia maudhui ya kidijitali nchini Kenya.
William Getumbe sasa anasalia huru kuendeleza kazi yake ya muziki na utayarishaji wa video mitandaoni bila masharti ya leseni zisizoambatana na sheria.