Entertainment

KRG The Don Akanusha Uhusiano na Freemasons, Afafanua Alama Zake za Mitandaoni

KRG The Don Akanusha Uhusiano na Freemasons, Afafanua Alama Zake za Mitandaoni

Msanii wa muziki wa dansi na mjasiriamali nchini Kenya, KRG The Don, amevunja ukimya wake kuhusu tuhuma za muda mrefu zinazomhusisha na kundi la kificho la Freemasons. Akiwa kwenye mahojiano ya hivi karibuni, KRG alikanusha vikali madai hayo na kueleza sababu halisi ya kutumia alama zinazodaiwa kuwa za Freemason kwenye picha na mitandao yake ya kijamii.

KRG amesema kuwa watu wamekuwa wakitafsiri vibaya ishara anazotumia kwa sababu ya kukosa uelewa wa sanaa na mitindo ya kujieleza kupitia picha. Alisema kuwa alama hizo ni sehemu ya ubunifu wa kisanii na hazihusiani kwa vyovyote na imani au makundi ya kisiri.

 “Mimi si Freemason na sijawahi kuwa. Watu wanapenda kuhusisha mafanikio ya mtu na mambo ya ajabu ajabu. Nimefanya kazi kwa bidii, sihitaji kutumia njia za mkato. Hizo ishara ni style tu, ni photography na creativity, si uchawi,” alisema KRG.

Kwenye picha nyingi zake mtandaoni, KRG ameonekana akitumia ishara kama kuweka mikono kwa mtindo wa pembetatu au kufunika jicho moja, alama ambazo kwa muda mrefu zimehusishwa na Freemason au kundi la Illuminati. Lakini KRG anasema hayo ni mitindo ya upigaji picha ambayo wasanii wengi duniani hutumia ili kuvutia mashabiki.

Aidha, msanii huyo alieleza kuwa kuna watu wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza propaganda na kueneza hofu kuhusu maisha ya watu mashuhuri bila ushahidi wowote.

“Sio kila kitu unachoona Instagram ni kiashiria cha mambo ya ajabu. Watu wengi wananitazama kama mfano wa mafanikio, lakini badala ya kujifunza, wanabuni stori za kunivuruga. Wacha waendelee kuongea, mimi naendelea kusonga mbele,” aliongeza.

KRG The Don ni mmoja wa wasanii waliopiga hatua kubwa katika tasnia ya muziki nchini Kenya, na pia amejizolea umaarufu kutokana na maisha ya kifahari anayoyaonyesha mitandaoni. Mafanikio haya yamekuwa chanzo cha uvumi mwingi kuhusu maisha yake ya binafsi, ikiwa ni pamoja na madai ya kujiunga na Freemasons ili kufanikisha ndoto zake.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, msanii huyo ameweka mambo wazi na kuwahakikishia mashabiki wake kuwa mafanikio yake yanatokana na juhudi halali, si imani au makundi ya kisiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *