
Mchekeshaji maarufu wa Kenya, Eric Omondi, ameonesha tena moyo wake wa huruma baada ya kusaidia kuchangisha zaidi ya KSh 800,000 kwa ajili ya Nyanya mmoja kutoka Homa Bay aliyevutia hisia za Wakenya kwa kubeba kuku hadi shuleni kama njia ya kulipa ada ya wajukuu wake.
Tukio hilo lilivuma mitandaoni baada ya picha na video za bibi huyo kusambaa, zikionyesha akijaribu kumkabidhi mwalimu kuku wawili kama sehemu ya malipo ya karo ya wajukuu wake. Kitendo hicho kiligusa mioyo ya Wakenya wengi, kutokana na hatua ya Nyanya huyo kutumia kile kidogo alichonacho kuhakikisha wajukuu wake wanaendelea na masomo.
Eric Omondi, kupitia kampeni yake ya “Sisi kwa Sisi,” aliongoza harakati za kuchangisha pesa kwa ajili ya familia hiyo. Ndani ya muda mfupi, mchango wa zaidi ya shilingi laki nane uliweza kukusanywa kupitia mitandao na michango ya moja kwa moja.
“Hili ni jambo lililoniathiri sana moyoni. Mama huyu alitoa kila alichonacho kwa ajili ya elimu ya wajukuu wake. Ni jukumu letu kama Wakenya kuhakikisha watoto hawa wanapata fursa ya kuendelea na masomo bila kikwazo,” alisema Eric Omondi kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Kwa sasa, familia hiyo imepokea msaada huo mkubwa wa kifedha, ambao mbali na ada ya shule, pia utawasaidia katika mahitaji mengine ya msingi kama chakula, mavazi, na makazi bora.
Wakenya wengi wamepongeza hatua hiyo ya Eric Omondi, wakimtaja kuwa mfano wa kuigwa kwa kutumia umaarufu wake kuleta mabadiliko chanya katika jamii.