Entertainment

King Kaka Afichua Siri ya Kuweza Kusawazisha Majukumu ya Uongozi, Muziki na Upishi

King Kaka Afichua Siri ya Kuweza Kusawazisha Majukumu ya Uongozi, Muziki na Upishi

Msanii maarufu wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Kennedy Ombima almaarufu King Kaka, amewashangaza mashabiki wake kwa mara nyingine baada ya kufichua jinsi anavyoweza kusawazisha majukumu yake mengi, akiwa Mkurugenzi Mtendaji (CEO), Mkurugenzi wa miradi, msanii wa muziki na hivi karibuni, mpishi (chef).

Katika mahojiano maalum, King Kaka alieleza kuwa utaratibu madhubuti, nidhamu ya hali ya juu, na moyo wa kujifunza ndiyo nguzo kuu zinazomsaidia kudhibiti maisha yake yenye shughuli nyingi.

“Watu wengi hufikiri ni ngumu, lakini nikikupenda kitu, utakipa muda. Mimi hupanga siku yangu kwa makini, kuna muda wa familia, kazi, na burudani,” alisema.

Mbali na kuendesha kampuni yake ya usimamizi wa wasanii na miradi ya kijamii, King Kaka bado anaendelea kutoa muziki wa kiwango cha juu na sasa ameanza safari mpya ya upishi, akionyesha ujuzi wake jikoni kupitia mitandao ya kijamii. Alisema kuwa mapishi ni moja ya njia zake za kujieleza na kupumzika.

“Upishi ni sanaa kama muziki. Ukiwa jikoni, unatengeneza ladha na hisia, ni kama kuandika beti kali kwenye wimbo,” aliongeza kwa tabasamu.

Katika hatua nyingine, amefichua kuwa kwa sasa yuko kwenye mazungumzo na mchekeshaji Crazy Kennar kwa ajili ya kushirikiana kwenye mradi wa filamu. Amedokeza kuwa ndani ya mwaka huu, mashabiki wanaweza kutarajia uzinduzi wa filamu pamoja na mfululizo wa tamthilia (series) zitakazogusa maisha halisi na kutoa burudani ya hali ya juu.

Kwa King Kaka, mafanikio yanatokana na nidhamu, ratiba thabiti, na kutoruhusu presha ya nje kumzuia kufanya kile anachopenda. Anaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengi wanaotamani kuingia katika sekta mbalimbali na kufaulu bila kupoteza mwelekeo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *