
Msanii maarufu wa Uganda na Rais wa Umoja wa Wasanii (Uganda National Musicians Federation), Eddy Kenzo, ametangaza nia ya kuanzisha mazungumzo ya wazi na msanii mwenzake Azawi, ili kutatua tofauti zao za kisiasa ambazo zimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wanamuziki nchini humo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kenzo amesema kuwa tofauti hizo hazipaswi kuendelezwa kwa njia ya mivutano ya mitandaoni bali kupitia mazungumzo ya moja kwa moja na ya wazi, akibainisha kuwa anathamini mchango wa Azawi katika tasnia na anataka suluhisho la kudumu.
“Kama viongozi wa sanaa, ni jukumu letu kuonyesha mfano. Ningependa tuketi na kuzungumza hadharani ili tuweze kuelewana na kusaidia kuunganisha tasnia yetu,” alisema Kenzo.
Wito huo wa Kenzo umepokelewa kwa hisia mseto mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakipongeza hatua hiyo kama ishara ya utu uzima na uongozi wa kweli, huku wengine wakimtaka aonyeshe vitendo zaidi badala ya maneno.
Kwa sasa, bado haijajulikana iwapo Azawi atakubali mwaliko huo wa mazungumzo ya hadharani, lakini mashabiki wengi wana matumaini kwamba tofauti hizo zitatatuliwa kwa njia ya amani na kwa manufaa ya sekta ya muziki nchini Uganda.
Taarifa hii inakuja baada ya Azawi kumkosoa hadharani mara kadhaa, akimtuhumu Kenzo kwa kushindwa kutumia nafasi yake ya uongozi kutetea masilahi ya wasanii na raia wa Uganda kwa ujumla. Azawi amekuwa akieleza kuwa Kenzo amekuwa kimya katika masuala muhimu yanayohitaji sauti ya msanii mwenye ushawishi kama yeye.