Others

Eddy Kenzo Apuzilia Mbali Madai ya Bebe Cool ya Kudhibiti Muziki

Eddy Kenzo Apuzilia Mbali Madai ya Bebe Cool ya Kudhibiti Muziki

Msanii nyota wa Uganda, Eddy Kenzo, ameibuka na kauli kali dhidi ya madai ya Bebe Cool kwamba yeye hudhibiti namna nyimbo zinavyopigwa kwenye redio na runinga nchini humo. Kenzo, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kimataifa kutoka Afrika Mashariki, amesema Bebe Cool hana ushawishi mkubwa kama anavyodai.

“Bebe Cool hana uwezo wa kudhibiti airplay kama anavyodhani. Sisi tulipata mafanikio makubwa wakati yeye bado yupo kwenye tasnia, kwa hiyo kauli zake hazina uzito wowote,” alisema Kenzo katika mahojiano na msanii Vampino.

Kauli hii ni majibu ya moja kwa moja kwa matamshi ya Bebe Cool aliyotoa mwezi Aprili, ambapo alijisifu kuwa ana ushawishi mkubwa kwenye vituo vya habari na anaweza kuzuia wimbo wowote usipigwe Uganda.

“Mimi si rafiki tu wa DJs, bali pia wa wamiliki wa vituo vya redio na TV. Naweza kuamua wimbo gani usipigwe popote nchini,” alisema Bebe Cool awali, akidai wasanii wachanga wanafaa kumheshimu kama mlezi wa tasnia.

Lakini kwa Eddy Kenzo, mafanikio hayatokani na upendeleo au vitisho vya watu maarufu bali kutokana na bidii, kipaji na kujituma kwa msanii binafsi.

“Wasanii wapya wasihangaike na matamshi kama haya. Wajikite kwenye kazi yao. Mafanikio hayaletiwi na maneno ya mtu bali kazi nzuri,” alisisitiza Kenzo.

Bifu hili la kauli kati ya mastaa hawa wawili linaashiria mvutano mkubwa wa ushawishi ndani ya tasnia ya muziki nchini Uganda, huku mashabiki wakigawanyika kati ya kuunga mkono upande wa Kenzo au Bebe Cool. Lakini kwa sasa, Kenzo ameweka wazi msimamo wake kwamba hana muda wa kuendekeza maneno yasiyo na msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *