
Rapa Tory Lanez, ambaye jina lake halisi ni Daystar Peterson, ameripotiwa kuhamishwa kutoka Gereza la California Correctional Institution lililopo Tehachapi, baada ya tukio la kushambuliwa na kuchomwa kisu mara 14.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na tukio hilo, Lanez alivamiwa ndani ya gereza hilo na kushambuliwa katika tukio linalodaiwa kuhusiana na migogoro ya magenge ya uhalifu, hasa kundi la Bloods. Ingawa majeraha aliyoyapata hayakuwa ya kutishia maisha, shambulio hilo limezua hofu kubwa kuhusu usalama wake akiwa gerezani.
Baada ya tukio hilo, rapa huyo alihamishiwa katika Gereza la North Kern State Prison, lililoko Delano, California, kwa lengo la kumlinda dhidi ya mashambulizi zaidi. Uhamisho huo unatajwa kufanyika haraka mara baada ya shambulio hilo.
Tory Lanez anatumikia kifungo cha miaka 10 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga risasi msanii mwenzake Megan Thee Stallion mwaka 2020, tukio ambalo lilizua gumzo kubwa katika tasnia ya burudani ya Marekani.
Hata hivyo, Idara ya Magereza na Marekebisho ya Tabia ya Jimbo la California haijatoa taarifa rasmi kuthibitisha tukio hilo au sababu za uhamisho, ikitaja sababu za faragha na usalama wa wafungwa.
Mashabiki na wafuasi wa rapa huyo sasa wanasubiri taarifa rasmi kuhusu hali yake ya afya na hatima ya kesi au uchunguzi wowote unaoweza kufunguliwa kutokana na tukio hilo la kushangaza.