Entertainment

Bahati Atangaza Ndoa na Diana Marua Mwaka 2026

Bahati Atangaza Ndoa na Diana Marua Mwaka 2026

Msanii nyota wa muziki nchini Kenya, Bahati, amewapa mashabiki wake habari ya kusisimua baada ya kuashiria kuwa hatimaye anapanga kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Diana Marua, mwaka ujao. Kupitia ujumbe wa hisia aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Bahati alifichua kuwa mwaka 2026 utakua wa kipekee kwao, kwani wataadhimisha miaka 10 ya kuwa pamoja.

Katika chapisho lake, Bahati alimweleza Diana kuwa amekuwa mvumilivu kwa miaka yote, akiahidi kuwa wakati wao wa kusherehekea upendo wao kwa njia ya ndoa umefika. Akitumia hashtagi ya #SikuKuuYaBahati, Bahati alionekana kuelekeza maandalizi ya tukio kubwa ambalo linaweza kuwa harusi yao rasmi.

“Mpenzi wangu mrembo @Diana_Marua, najua tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu ndoa yetu. Mwaka ujao tutatimiza miaka 10 pamoja. Najua inaonekana kama ni muda mrefu lakini usiali, #SikuKuuYaBahati itakuwa ya kipekee.”

Bahati pia alielezea jinsi harusi ya msanii wa Bongo Fleva kutoka Tanzania, Juma Jux, ilivyomgusa na kumtia moyo kama mwanaume. Akitumia alama ya reli #JP2025, alikiri kuwa harusi hiyo ilimfundisha thamani ya kumpenda na kumheshimu mwanamke.

 “#JP2025 imenifundisha jinsi mwanaume anavyopaswa kumthamini na kumuenzi yule anayempenda. Kaka yetu wa Afrika Mashariki, Jux, ametuheshimisha. Hongera sana kaka yangu @Juma_Jux na mrembo @its.priscy. Nathibitisha wazi kuwa mimi ndiye ninayefuata #BD2025.”

Baada ya chapisho hilo, mashabiki walimiminika kwenye sehemu ya maoni wakionyesha furaha, wakitoa pongezi na pia kuomba kuhudhuria harusi hiyo. Wengi walieleza kuwa wamekuwa wakisubiri muda mrefu kuona Bahati akimvalisha Diana pete ya ndoa madhabahuni.

Ikiwa mipango hiyo itatimia, basi mwaka 2025 huenda ukawa mwaka wa kihistoria kwa Bahati na Diana, na huenda pia tukashuhudia harusi mojawapo ya kifahari zaidi katika burudani ya Afrika Mashariki.