
Klabu ya Arsenal imeanza mazungumzo rasmi na wakala wa mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres, jijini Lisbon, Ureno. Lengo la mazungumzo hayo ni kuhakikisha wanamnasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden, ambapo tayari Arsenal imewasilisha ofa ya Pauni milioni 59.
Ingawa mazungumzo bado yanaendelea, Sporting imeonyesha utayari wa kumwachia Gyokeres kwa kiasi hicho, kutokana na heshima aliyoionyesha klabu hiyo kwa kukataa kuondoka katika dirisha la usajili la majira ya baridi, licha ya kupokea ofa kubwa kutoka klabu mbalimbali.
Gyokeres, ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2028, amekuwa na msimu wa kuvutia akiwa na Sporting, akifunga mabao 54 na kutoa asisti 13 katika mechi 52 za michuano yote. Arsenal inamtazama kama chaguo bora kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa msimu ujao.