Tech news

Meta Yaongeza Muda wa Instagram Reels Kwa Dakika 20

Meta Yaongeza Muda wa Instagram Reels Kwa Dakika 20

Kampuni ya Meta kupitia jukwaa lake la Instagram, imetangaza rasmi kuongezwa kwa muda wa video za Reels kutoka dakika 3 hadi dakika 20, hatua ambayo inachukuliwa kama mabadiliko makubwa ya kuvutia watumiaji wanaopendelea maudhui marefu zaidi.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na timu ya Instagram, imeelezwa kuwa ongezeko hili la muda linakusudia kuwapa watumiaji, hasa watoa maudhui (content creators), nafasi zaidi ya kueleza simulizi zao, kuwasilisha kazi za ubunifu, na kushindana moja kwa moja na majukwaa mengine kama YouTube na TikTok, ambayo tayari yanaunga mkono video ndefu.

“Tumewasikiliza watumiaji wetu na tunaelewa kuwa ubunifu haupaswi kufungwa na kikomo cha muda mfupi,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Instagram.

Hii ni fursa mpya kwa wanaburudani, walimu mtandaoni, wablogu wa safari na wapishi, ambao awali walilazimika kukata vipande vya maudhui yao au kutumia majukwaa mengine kwa video ndefu. Sasa, video za burudani, elimu, mahojiano mafupi, na mfululizo wa hadithi zinaweza kusimuliwa kikamilifu ndani ya Reels.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mitandao ya kijamii wameonya kuwa mabadiliko haya huenda yakahitaji pia maboresho katika muundo wa uwasilishaji wa Reels, ikiwemo jinsi wanavyopatikana kwenye “feed” na uhusiano wake na algorithm ya kupendekeza maudhui.

Instagram Reels ilizinduliwa mwaka 2020 kama jibu la Meta kwa ongezeko la umaarufu wa video fupi kupitia TikTok. Kwa muda mrefu, Reels zimekuwa na kikomo cha sekunde 15, baadaye dakika 1, na kisha dakika 3 kabla ya hatua hii ya sasa ya kuongeza hadi dakika 20.

Kwa hatua hii mpya, Instagram inaonesha dhamira ya kuendelea kuwa jukwaa bunifu, linalojibadilisha kulingana na mahitaji na mitindo ya kisasa ya maudhui mtandaoni.