
Msanii wa muziki wa R&B kutoka Kenya, Victoria Kimani, hatimaye amejibu ukosoaji ulioibuka baada ya mahojiano yake kwenye Mic Cheque Podcast, ambako alitoa kauli iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni dongo kwa msanii nyota wa Tanzania, Diamond Platnumz.
Katika mahojiano hayo, Kimani alidai kuwa kuna Rolls Royce ya rangi ya buluu inayodaiwa kuwa ya bandia, kauli ambayo iliwafanya mashabiki wengi kuamini kuwa alikuwa akimlenga Diamond, ambaye hivi majuzi alijivunia kumiliki gari hilo la kifahari.
Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano na mtangazaji Milard Ayo, Victoria Kimani alikanusha madai hayo kwa kusisitiza kuwa hakuwa amemtaja mtu yeyote kwa jina.
“Sikutaja jina la mtu yeyote… acheni. Nilisema nilichosema, haikuwa maana ya ndani,” alisema Kimani kwa msisitizo.
Kauli hiyo ya Kimani imeibua mjadala mkali mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimtetea kwa kusema ana uhuru wa kutoa maoni yake, na wengine wakimtaka awe makini na matamshi yake, hasa inapohusiana na wasanii wengine wakubwa wa Afrika Mashariki.
Diamond Platnumz hajatoa tamko rasmi kuhusiana na madai hayo, huku baadhi ya mashabiki wake wakimtetea vikali kwenye mitandao ya kijamii.
Mashabiki sasa wanasubiri kuona iwapo kutakuwa na mwendelezo wa mvutano huu au kama pande zote zitapuuza na kuendelea na kazi zao za kisanaa.