Entertainment

Bien wa Sauti Sol Aibuka na Kuku Hai Katika Show ya DJ AG London

Bien wa Sauti Sol Aibuka na Kuku Hai Katika Show ya DJ AG London

Msanii mashuhuri wa kundi la Sauti Sol, Bien-Aimé Baraza, ameibua mshangao na vicheko mitandaoni baada ya kuonekana akitumbuiza katika onyesho la mtaa la DJ AG maarufu jijini London huku akibeba kuku hai mikononi.

Tukio hilo lilifanyika katika eneo la King’s Cross, ambapo DJ AG huandaa matukio ya kipekee ya muziki ya mtaani, yanayopata sifa kwa ubunifu na mvuto wake wa kipekee. Bien sasa amejiunga rasmi na orodha ya watu maarufu waliowahi kushiriki au kuonekana kwenye onesho hilo, akiwemo Ed Sheeran, Will Smith, Rita Ora, Flavour, Demarco, na hivi karibuni Diamond Platnumz.

Katika video iliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, Bien alionekana akicheza kwa hisia na kuimba huku akiwa amembeba kuku – jambo lililowafanya mashabiki washangae, wengine wakicheka, wakitafsiri tukio hilo kama mvuto wa Kiafrika iliyoongeza ladha ya kipekee kwenye burudani hiyo.

DJ AG, anayejulikana kwa kuandaa street sets zinazolenga kuonyesha vipaji vya wasanii maarufu pamoja na wachanga, ameendelea kuvutia macho ya dunia kwa namna anavyounganisha muziki, mitandao ya kijamii na utamaduni wa mitaani. Onyesho hilo limeibuka kuwa jukwaa wazi la ubunifu na maonyesho yasiyo na mipaka.

Mashabiki wa Bien na kundi la Sauti Sol wamepongeza kitendo hicho kama ishara ya ubunifu wa hali ya juu na utangazaji wa utamaduni wa Kiafrika katikati ya jiji la London.

“Bien ni msanii anayeweza kuwasiliana na hisia za watu, na pia ana kipaji cha kuleta vichekesho. Hii ya kuku imeweka historia nyingine kabisa!” aliandika shabiki mmoja kwenye X (zamani Twitter).

Kwa sasa, mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona ni nani mwingine maarufu atakayejiunga na DJ AG katika street shows zake zijazo