
Mwanamuziki maarufu wa hip hop, Nicki Minaj, ameibua shinikizo kwa rapa na mwekezaji, Jay-Z, akidai kuwa anamdai kati ya dola milioni 100 hadi 200 baada ya kuuza mtandao wa kusikiliza muziki wa TIDAL mwaka 2021.
Katika madai haya ambayo yamezua gumzo mitandaoni, Nicki amesema kuwa alikuwa mmoja wa wasanii wa awali kumiliki sehemu ya mtandao huo na alifanya juhudi kubwa zaidi za kuitangaza TIDAL, ikiwemo kuliko msanii mwenzake, Beyoncé, wakati wa uzinduzi wa mtandao huo.
“Nilipambana sana kutangaza TIDAL, zaidi hata ya Beyoncé,” alisema Nicki.
Nicki anadai kuwa wakati Jay-Z aliuza mtandao wa TIDAL kwa kampuni ya Square, inayomilikiwa na Jack Dorsey aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Twitter, kwa kiasi cha dola milioni 300, wasanii wenzake walilipwa kati ya dola milioni 8 hadi 9 kila mmoja, lakini yeye hakuambulia hata senti.
Zaidi ya hayo, Nicki amesema alipokea ofa ya dola milioni 1 (takriban Shilingi bilioni 2.6) ili kutuliza madai haya, lakini alikataa.
“Nilipewa ofa ya dola milioni moja ili ninyamaze, lakini sikuikubali. Mashabiki wangu wanastahili kujua ukweli,” alisema Nicki.
Madai haya yamepokelewa kwa msisimko mkubwa, huku mashabiki wake, maarufu kama Barbz, wakimpongeza kwa kuonyesha maadili ya kuhimiza uwazi na haki, hasa kwa kuwa Nicki alichangia kwa kiasi kikubwa katika kuifanya TIDAL kuwa mtandao maarufu.
Kwa historia, Jay-Z alinunua TIDAL mwaka 2015 kwa dola milioni 56 na baadaye kuuza hisa nyingi za mtandao huo kwa kampuni ya Square kwa dola milioni 297 (kama Shilingi bilioni 689+).
Wasanii wengine wamiliki wa mtandao huo ni pamoja na Alicia Keys, Beyoncé, J. Cole, Kanye West, Lil Wayne, Rihanna, T.I, pamoja na Nicki Minaj mwenyewe.
Madai haya yanazua mjadala mzito katika tasnia ya muziki na uwekezaji, huku wengi wakisubiri maelezo rasmi kutoka kwa Jay-Z na kampuni ya Square kuhusu madai ya Nicki Minaj.