
Mchekeshaji maarufu Eric Omondi ameibua hisia mseto mitandaoni baada ya kutoa kauli fupi lakini nzito kufuatia agizo la Rais William Ruto, linalowataka maafisa wa usalama kuwafyatulia risasi mguuni wale wanaohusika na uharibifu wa mali ya umma.
Akiwa kwenye Ibada ya mazishi ya marehemu Boniface Mwangi Kariuki, Eric alionesha kusikitishwa na mwelekeo wa kisiasa na kijamii nchini, akisema kuwa taifa linahitaji maombi zaidi ya chochote kingine kwa sasa. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Rais kutoa agizo hilo akiwa katika hafla ya hadhara.
Agizo la Rais limezua mjadala mkubwa nchini, huku baadhi ya wananchi na wanaharakati wa haki za binadamu wakieleza wasiwasi wao kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na uwezekano wa kukiukwa kwa haki za raia.
Eric Omondi, ambaye amejitokeza mara kadhaa kuikosoa serikali na kuongoza harakati za kijamii, anaonekana kuashiria hali ya taharuki na sintofahamu inayozidi kushika kasi nchini. Wafuasi wake wengi wamelitafsiri tangazo lake kama kilio cha kutafuta amani na busara katika uongozi wa taifa.
Mjadala kuhusu agizo la Rais unaendelea kushika kasi, huku wadau mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusu uhalali, athari na mwelekeo wa hatua hiyo kwa mustakabali wa haki za binadamu na demokrasia nchini.