LifeStyle

Mwanamitindo Liebe Kiki Aachana na Bleaching, Ahamasisha Kujikubali

Mwanamitindo Liebe Kiki Aachana na Bleaching, Ahamasisha Kujikubali

Mwanamitindo na influencer maarufu, Liebe Kiki, amefunguka kuhusu safari yake ya kurejesha rangi yake halisi ya ngozi baada ya kutumia kwa muda mrefu bidhaa za kubadilisha rangi.

Katika taarifa yake kupitia Instagram, Kiki alieleza kuwa yuko kwenye hatua za mwisho za kuondoa athari za bleaching na kufichua kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kuanza mchakato huo ilikuwa ni majeraha ya kihisia aliyopitia akiwa mtoto.

Kiki alisema kuwa alipitia changamoto nyingi za kiakili na kihemko ambazo zilisababisha kujitafuta kwa kina, hali iliyompelekea kufanya maamuzi ambayo baadaye aligundua yalikuwa ya kujeruhi nafsi yake. Aidha, alieleza kuwa ujasiri wa kueleza hadharani kuhusu mabadiliko ya ngozi ni sehemu ya safari yake ya kujikubali.

Mashabiki wake wamepongeza hatua yake hiyo wakisema ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengi wanaojikuta kwenye shinikizo la mabadiliko ya mwonekano kutokana na hali ya kijamii au familia. Ushuhuda wake umetajwa kuwa wa kuhamasisha watu wengi kuukubali uhalisia wao na kutafuta utilivu wa roho badala ya suluhisho za nje.

Suala la kubadili rangi ya ngozi limeendelea kuibua mijadala mikali mtandaoni, hasa kuhusu athari zake kiafya na kiakili. Kwa hatua yake ya kujieleza kwa uwazi, Liebe Kiki sasa anachukuliwa kama sauti ya mabadiliko na mfano wa kuigwa katika kujikubali na kujipenda jinsi ulivyo.