
Kampuni ya WhatsApp imeanza rasmi majaribio ya kipengele kipya kitakachowezesha makundi (Groups) kuwa na sehemu maalum ya Status, sawa na jinsi watumiaji wa kawaida wanavyoweka status binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na majaribio hayo, mabadiliko haya yanalenga kuongeza mwingiliano wa kijamii ndani ya Groups, kwa kutoa nafasi kwa wanachama wa kundi kushiriki maudhui ya muda (status) yanayoonekana na members pekee wa group hilo.
Kupitia kipengele hiki, kila Group kitakuwa na sehemu maalum ya Status, ambapo members wataweza kuchapisha status zao. Tofauti na status za kawaida, hizi hazitaonekana kwa watumiaji walio nje ya Group, hivyo kuongeza usiri na umakini wa mawasiliano ndani ya kundi. Aidha, WhatsApp imetoa uwezo kwa admin wa Group kudhibiti nani anaruhusiwa kuweka Status ama kutoa ruhusa kwa members wote, au kuweka kuwa admin tu ndiye anayeweza kuchapisha.
Kipengele hiki kinatazamiwa kuongeza idadi ya views kwenye Status, kwa kuwa watumiaji sasa wataweza kushiriki status zao kwa watu wengi zaidi waliopo kwenye Group moja, hata kama si marafiki wa moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi.
Hatua hii ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za WhatsApp kuboresha huduma zake kulingana na tabia na mahitaji ya watumiaji wake, na kuifanya kuwa zaidi ya jukwaa la ujumbe ikichukua nafasi ya kuwa sehemu ya kijamii inayotoa fursa za kushirikishana zaidi.
Kwa sasa, kipengele hiki kiko katika hatua ya majaribio, na kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi kwa watumiaji wote katika toleo lijalo la app hiyo baada ya tathmini ya awali kukamilika.