
Msanii mkongwe wa muziki wa Genge, Nonini, anakumbwa na ukosoaji mkali mitandaoni baada ya kupakia video ya nyuma ya pazia (behind-the-scenes) ya wimbo mpya kutoka kwenye albamu yake inayotarajiwa kuingia sokoni hivi karibuni.
Video hiyo, iliyochapishwa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), ilimuonesha Nonini akiwa studio akiimba kwa mtindo wake wa kipekee wa Genge huku akijaribu kuuchanganya na ladha za kisasa.
Katika video hiyo, Nonini anasikika akitoa mistari inayogusia maisha yake jijini Nairobi na changamoto alizopitia akiwa ughaibuni. Aliandika kwenye chapisho hilo kuwa wimbo huo ni wa mwisho katika albamu yake mpya, na kwamba muziki kwake ni taswira ya maisha yake binafsi.
Hata hivyo, badala ya kupokelewa kwa shangwe, video hiyo ilisambaa kwa kasi kutokana na mtindo wake wa uimbaji ambao wengi waliuelezea kama wa kizamani na usioendana na ladha ya muziki wa sasa. Watumiaji wengi wa X walimkosoa wakisema kuwa licha ya heshima yake kama mmoja wa waanzilishi wa muziki wa Genge nchini, Nonini anapaswa kubadilika ili kuwavutia wasikilizaji wa kizazi kipya.