
Kampuni ya teknolojia ya Apple, inatarajiwa kuzindua toleo jipya la iPhone ambalo linatajwa kuwa tofauti kabisa na matoleo ya awali. Taarifa kutoka kwa vyanzo vya karibu na kampuni hiyo zinaeleza kuwa iPhone hiyo mpya itakuwa na vioo viwili, hatua ambayo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wapenzi wa teknolojia duniani.
Kioo cha kwanza kitakuwa kikubwa na cha ndani, kama ilivyo kawaida kwa simu za iPhone. Lakini kipya zaidi ni kioo cha nje ambacho kitakuwa na ukubwa wa inchi 5.5, sawa kabisa na simu ya kawaida. Kioo hicho cha nje kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuonyesha taarifa muhimu kama muda, ujumbe mfupi, arifa, na hata kutumia baadhi ya apps bila kulazimika kufungua kioo kikuu.
Hii ni mara ya kwanza kwa Apple kujaribu rasmi teknolojia ya simu yenye vioo viwili, teknolojia ambayo tayari imejaribiwa na makampuni kama Samsung kupitia simu zake za “foldable”. Tofauti na simu zinazokunjwa, iPhone hii mpya haikunjiki, bali inakuwa na kioo cha pili kwa matumizi ya haraka na ya nje.
Hadi sasa, Apple haijatoa tarehe rasmi ya uzinduzi wa iPhone hii, lakini matarajio ni kwamba itazinduliwa katika tukio kubwa la uzinduzi wa bidhaa za Apple ambalo hufanyika kila Septemba.