
Msanii kutoka Tanzania, Zuchu, amejitokeza na kukanusha vikali madai kwamba alipuuziwa na mashabiki wakati wa onyesho lake katika Uwanja wa Kasarani, wakati wa fainali za mashindano ya CHAN kati ya Morocco na Madagascar.
Ripoti zilizosambaa mitandaoni zilisema kuwa baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwanjani walionekana kuimba wimbo wa taifa la Kenya wakati Zuchu alipokuwa akiendelea na maonesho jukwaani, hali iliyotafsiriwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao kama ishara ya kutompa usikivu au heshima anayostahili.
Kupitia mitandao ya kijamii, hususan Instagram, Zuchu alikanusha madai hayo akisisitiza kuwa video zilizozagaa mtandaoni zimehaririwa kwa nia ovu ya kueneza taarifa potofu. Alieleza kuwa onyesho hilo lilirushwa moja kwa moja (live) na linapatikana kwa ukamilifu kwenye YouTube, hivyo kama tukio hilo lingetokea kweli, lingeonekana bayana kwenye rekodi ya moja kwa moja.
Hitmaker huyo wa Amanda ameendelea kusisitiza kuwa mafanikio ya kazi yake hayawezi kutikiswa na kauli za watu wachache mitandaoni, kwani chapa yake inasimamiwa na juhudi, maombi, na mashabiki wake wa kweli walioko ndani na nje ya Tanzania.
Tukio hilo, ambalo lilidaiwa kutokea wakati wa mechi kubwa ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), limezua mjadala mitandaoni huku baadhi ya mashabiki wakimtetea vikali Zuchu, wakisema alitoa burudani ya hali ya juu licha ya kelele za mtandaoni.