
Instagram imeanza kujaribu mfumo mpya wa Picture-in-Picture (PIP), ambao utawawezesha watumiaji wake kuendelea kutazama video za Reels hata baada ya kufunga app ya Instagram. Kwa kutumia teknolojia hii, watumiaji wataweza kufanya shughuli nyingine kwenye simu zao huku bado video ikiendelea kuonekana kwenye kona ya skrini.
Kwa mfano, unaweza kutazama Reel huku ukiandika ujumbe kwenye WhatsApp, kusoma meseji, kutumia browser au hata ukiwa kwenye home-screen ya simu yako. Hii ni hatua kubwa kwa Instagram katika kuongeza urahisi wa kutumia app na kuwapa watumiaji wake uwezo wa multitasking bila kukatizwa na hitaji la kubaki ndani ya app muda wote.
Kwa sasa, hii ni huduma ya majaribio na inapatikana kwa watumiaji wachache tu. Hata hivyo, Instagram imethibitisha kuwa mfumo huu mpya utaanza kupatikana kwa watumiaji wote hivi karibuni.
Maboresho haya yanaashiria mwelekeo mpya wa Instagram wa kufanya matumizi ya video kuwa rahisi zaidi na kuendana na mahitaji ya watumiaji wa kisasa wanaotaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.