Mwanamitandao aliyegeukia muziki,Diana B, ametangaza rasmi kurejea kwenye muziki baada ya ukimya wa miaka miwili wa kutoachia wimbo wowote.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diana B amedokeza kuwa leo atawazawadia mashabiki wimbo mpya unaoitwa “Bibi Ya Tajiri”. Akiwa mwenye bashasha, ameeleza kuwa kipindi chote cha miaka miwili hakukuwa cha kupumzika bali cha kufanya kazi kwa bidii ili kujijenga.
Diana ambaye amekuwa akijulikana kwa kuonyesha maisha yake ya kifahari pamoja na mume wake msanii Bahati, amejinasibu kuwa jitihada zake zimezaa matunda na kwamba kwa sasa anajivunia kuwa tajiri, kauli ambayo pia ndiyo jina la single yake mpya.
Ujumbe huo umewasha moto wa shauku miongoni mwa mashabiki wake, wengi wakimpongeza kwa kurudi kwenye muziki na wengine wakingojea kuona kama wimbo huo utadhihirisha hadhi ya kifahari na mafanikio anayojigamba nayo.
Mashabiki na wadau wa muziki sasa wanasubiri kwa hamu ujio wa “Bibi Ya Tajiri”, ambao unatarajiwa kuwa mwanzo mpya wa safari ya Diana katika tasnia ya burudani.