Sports news

Timu ya Kenya ya Voliboli ya Wenye Ulemavu wa Kusikia Yalenga Nishani Tokyo

Timu ya Kenya ya Voliboli ya Wenye Ulemavu wa Kusikia Yalenga Nishani Tokyo

Timu ya taifa ya akinadada ya voliboli ya wachezaji wasiokuwa na uwezo wa kusikia ina matumaini makubwa ya kutwaa nishani katika Michezo ya Olimpiki kwa wachezaji wenye ulemavu wa kusikia (Deaflympics) yatakayofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia tarehe 15 hadi 26 Novemba mwaka huu.

Licha ya kupangwa katika kundi gumu, timu hiyo ya Kenya imesisitiza kuwa iko tayari kupambana na wapinzani wao wakubwa Italia, Marekani na wenyeji Japan waliotengewa kundi A pamoja nao. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kuwakilishwa katika mchezo wa voliboli kwenye michezo hiyo ya Olimpiki kwa wenye ulemavu wa kusikia.

Mbali na voliboli, Kenya pia itashiriki kwa mara ya kwanza katika michezo mingine kadhaa ikiwemo tenisi, tenisi ya mezani, mashindano ya baiskeli, uogeleaji, bowling na badminton. Aidha, timu za Kenya zitawakilisha taifa kwenye riadha, soka la akinadada, mpira wa mikono kwa wanaume, gofu na mpira wa kikapu kwa akinadada.

Kenya ilipata nafasi ya moja kwa moja kushiriki katika voliboli baada ya kutambuliwa kama timu bora barani Afrika katika mchezo huo, hatua inayotoa matumaini makubwa kwa wachezaji na mashabiki wa michezo ya walemavu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *