Entertainment

Bahati Aomba Msamaha Hadharani Baada ya Ukosoaji Mkubwa wa Mashabiki

Bahati Aomba Msamaha Hadharani Baada ya Ukosoaji Mkubwa wa Mashabiki

Msanii wa muziki mwenye utata kutoka Kenya, Bahati, amelazimika kuomba msamaha hadharani kufuatia wimbi la ukosoaji alilopokea kutokana na maudhui yake mapya tangu arejee kwenye muziki.

Kupitia video aliyoipakia kwenye mitandao ya kijamii, Bahati ameeleza kuwa amepokea simu na jumbe nyingi kutoka kwa marafiki wa karibu, mashabiki, wachungaji, na hata watu wasiowajua, wakionesha kutoridhishwa na mwelekeo wa kazi zake za hivi karibuni. Amesema hakutaka kujibu kwa hasira au hisia kwa kuwa anawaheshimu wote, na badala yake aliamua kuzungumza nao moja kwa moja kutoka moyoni.

Bahati amesema kuwa anatambua amewaudhi baadhi ya watu kutokana na mienendo na maudhui ya muziki wake wa sasa, hasa baada ya kurejea na wimbo wake mpya Set It. Ameeleza kuwa lengo lake halikuwa kuwakera, bali kuonyesha ubunifu wake kama msanii anayekua na kubadilika.

Msanii huyo ameongeza kuwa anatambua umuhimu wa mashabiki wake, familia, na washirika wake wa karibu, akiwashukuru kwa kumuunga mkono kwa kipindi cha miaka 10 kwenye muziki. Kwa mujibu wake, mafanikio yake yamechangiwa zaidi na upendo na uvumilivu wa mashabiki wake kuliko uwezo binafsi wa uimbaji.

Bahati pia ametumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa wote aliowakera, akisema yeye ni binadamu anayejifunza kila siku. Amesisitiza kuwa anakubali kurekebishwa lakini pia anahitaji maombi na msaada wa wale wanaomuamini.

Aidha, ameahidi kutorudia makosa ya kutayarisha maudhui yanayokwenda kinyume na maadili ya jamii, akisema anajitathmini upya ili kuhakikisha kazi zake za baadaye zinabeba ujumbe chanya na wenye manufaa kwa mashabiki wake.

Kauli yake inakuja mara baada ya kuachia wimbo wenye utata uitwao Set It, ambao umeonekana kuhamasisha ngono na kuibua mjadala mkali mitandaoni. Mbali na hilo, Bahati pia alichapisha misururu ya video zinazomuonyesha akiwa amevalia chupi na nyingine akinywa mvinyo alioshea miguu ya mkewe, Diana Marua, jambo lililowakera mashabiki wengi waliomkosoa kwa kupoteza maadili aliyojulikana nayo awali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *