Mwanamuziki mkongwe nchini Uganda, Bebe Cool, ameibuka tena na ukosoaji mkali dhidi ya Bobi Wine na chama chake cha National Unity Platform (NUP), akidai kuwa upinzani huo hauna uwezo wala maandalizi ya kutosha kuongoza Uganda.
Kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini humo, Bebe Cool ameeleza kuwa kutofanikiwa kwa NUP kuteua wagombea katika maeneo kadhaa ya uchaguzi ni ishara tosha ya kukosa maandalizi.
Bosi huyo wa Gagamel, amesema licha ya NUP kuwa na takribani wabunge 57 katika Bunge la sasa, iliweza kuwasimamisha wagombea 297 pekee, huku NRM ikisimamisha zaidi ya wagombea 500, akiongeza kuwa tayari wabunge kumi wa NRM wamepita bila kupingwa.
Kwa mtazamo wake, hali hiyo inaonyesha kuwa NUP haikuwa na watu wa kutosha wenye uwezo wa kugombea katika maeneo ambayo yalibaki wazi. Bebe Cool amesisitiza kuwa hali hii ni ishara kwamba Bobi Wine na timu yake bado wako mbali na kuelewa uhalisia wa siasa za kitaifa, akieleza kuwa upinzani huo unahitaji maandalizi zaidi.
Kwa mujibu wa Bebe Cool, ukosefu huo wa utayari unadhihirisha kuwa NUP inapaswa kujipanga upya ikiwa inataka kuwa na nafasi ya kushindana kwa ufanisi katika siku zijazo. Amedokeza kuwa huenda chama hicho kitapata nafasi bora zaidi katika mwaka wa 2031, endapo kitaongeza maandalizi na uwekezaji wa kisiasa.