Mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu nchini Kenya, Akothee, amejitokeza kutoa msimamo mkali, akimkinga kifua Mbunge wa EALA, Winnie Odinga dhidi ya kile anachokiita ubaguzi wa kisiasa.
Akothee amekemea vikali wale wanaomdhalilisha Winnie Odinga, binti ya hayati Raila Odinga, kwa kigezo cha kuwa hajaingia kwenye ndoa. Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Akothee, amesisitiza kuwa sifa za mtu katika siasa hazipaswi kuhukumiwa na hali yake ya ndoa.
Akizungumzia suala la ndoa, amesema kwa shauku kwamba ndoa haifai kuchukuliwa kama mafanikio, akidai kuwa taasisi hiyo ya ndoa ni kwa ajili ya wanawake ambao hawana mwelekeo wa maisha na ambao wanahitaji kuongozwa.
Akothee amewaonya vikali wanasiasa na wafuasi wao wanaotumia lugha chafu na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika ulingo wa siasa, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia akili, bidii, na mafanikio ya wanawake badala ya kuzingatia hali yao ya kibinafsi ya ndoa.
Mwanamama huyo amemalizia ujumbe wake kwa kusema kwamba hata kama watu hawakubaliani na mawazo ya kisiasa ya Winnie, wanapaswa kukosoa kwa staha na kuheshimu utu wake kama binadamu.