Msanii mwenye utata mkubwa nchini Uganda, Alien Skin, ametoa matamshi makali dhidi ya wasanii wanaoendelea kutumbuiza kwenye kampeni za Rais Yoweri Museveni baada ya kujiondoa kwenye misafara ya kampeni kutokana na malipo duni.
Akiwa jijini Kampala, Alien Skin amewakashifu wasanii hao, akisema juhudi zao hazina nguvu kwa sababu muziki wake ndio unaoamsha umati na kuongeza hamasa kwenye mikutano ya kisiasa. Anadai kuwa hata akiwa hayupo kwenye eneo la kampeni, nyimbo zake ndizo zinazoongoza na kutawala hewani, hali inayochangia kuvutia wafuasi wengi.
Alien Skin anasema kwa msingi huo, anapaswa kulipwa kwani muziki wake ndio unaotumika kuongeza namba za watu kwenye kampeni na kuleta nguvu kwenye mikutano hiyo.
Kauli hizi zinakuja siku chache baada ya video kusambaa mtandaoni ikimuonyesha Eddy Kenzo na wasanii wengine wakicheza wimbo wa Alien Skin katika mkutano wa Museveni huko mashariki mwa Uganda, huku Alien Skin mwenyewe akiwa hajahudhuria.