Mwanamuziki kutoka nchini Uganda, Irene Ntale, amezua mjadala mkali mtandaoni baada ya kutoa mtazamo wake kuhusu mgawanyo wa majukumu ya kifedha ndani ya ndoa.
Ntale ambaye juzi kati ameingia kwenye ndoa, amesema kuwa kwenye uhusiano ulio imara na uliopangika vizuri, mwanaume anapaswa kubeba majukumu yote makubwa ya kifedha, akisisitiza kuwa hilo ni hitaji la msingi katika kuleta uongozi na utulivu ndani ya familia.
Kwa mujibu wake, mwanaume ndiye anayepaswa kuhudumia gharama muhimu kama ada za shule, kodi ya nyumba, mafuta ya gari pamoja na matumizi makubwa ya nyumbani.
Hitmaker huyo wa Onkubirako, ameeleza kuwa jukumu la mwanamke halipaswi kuwa mzigo wa kulipia bili kubwa, lakini akawashauri wanawake kutojiingiza katika tabia ya kudai kila kitu au kuacha majukumu madogo yakisubiri wanaume.
Amesisitiza kuwa wanawake wanaweza kuchangia katika gharama ndogondogo ili kuimarisha ushirikiano wa kifamilia badala ya kuwa na mtazamo wa kutaka kusaidiwa kila jambo.
Aidha, Ntale ameonya kuwa pale mwanamke anapojitwika majukumu yote ya kifedha, kuna hatari ya baadhi ya wanaume kutumia mianya hiyo vibaya.