Kampuni ya Meta imefuta rasmi akaunti ya Instagram inayomilikiwa na mwanaharakati wa Marekani mwenye asili ya Tanzania na mkosoaji mkali wa serikali ya Rais Samia Suluhu, Mange Kimambi.
Mange amedai kuwa alipoteza kabisa akaunti yake yenye wafuasi zaidi ya milioni 2.7 siku ya Jumatano, Desemba 3, akisema hakuna dalili za kurejeshwa. Aidha, ameeleza kuwa amepigwa marufuku kutumia WhatsApp, ambayo pia inamilikiwa na Meta, hatua anayoiita jaribio la kumzuia kufikisha ujumbe kwa hadhira yake.
Wakati uo huo, mwanaharakati mwingine ambaye ni mkosoaji wa serikali, Maria Sarungi, ameripoti kuwa akaunti yake ya Instagram imekuwa ikikumbwa na shadow ban, hali inayosababisha wafuasi wake nchini Tanzania kushindwa kuona maudhui anayochapisha.
Mange na Sarungi wamekuwa miongoni mwa sauti zenye ushawishi mkubwa mtandaoni zinazokosoa kwa ukali utawala wa Rais Samia Suluhu, na hatua hizi kutoka Meta zimeibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kujieleza na usalama wa wanaharakati katika majukwaa ya kidijitali.