Msanii wa Bongo Fleva Marioo anatuhumiwa kutumia maroboti kupata views za wimbo wake mpya “Oluwa”, baada ya kazi hiyo kufikisha views milioni moja ndani ya siku mbili pekee tangu kuachiwa kwake.
Madai hayo yameibuka miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki mitandaoni, wakidai kasi ya kupanda kwa views hizo haieleweki kirahisi ikizingatiwa hali ya sasa ya soko la muziki nchini Tanzania.
Baadhi ya mashabiki wamehoji alipataje idadi hiyo kubwa ya watazamaji kwa muda mfupi, hasa wakati huu ambapo Watanzania wengi wanadaiwa kususia kazi za wasanii kufuatia kujihusisha kwao na siasa za uchaguzi zilizokumbwa na utata.
Aidha, wengine wamedai kuwa wimbo wa “Oluwa” hauonekani kwenye orodha ya nyimbo zinazovuma au trending nchini Tanzania, jambo lililozidi kuibua shaka kuhusu uhalali wa takwimu hizo. Mjadala huo unaendelea kushika kasi mitandaoni huku wengi wakisubiri kauli ya msanii huyo au timu yake ya usimamizi.