Mtayarishaji wa maudhui na mtangazaji wa redio, Azziad Nasenya, amewasuta vikali wakosoaji wanaoendelea kumshambulia mitandaoni kwa kile walichodai ni kubadilika kwa lafudhi (accent) yake ya lugha ya Kiingereza.
Azziad ameeleza kuwa lafudhi yake itaendelea kubadilika kadri anavyoendelea kukutana na tamaduni na jamii mbalimbali, na kwamba hakuna kiwango cha unyanyasaji au kejeli kitakachoweza kumkatisha tamaa.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Azziad amesema ana uwezo mkubwa wa kiakili na kisaikolojia (strong mental capabilities), hali inayomsaidia kustahimili shinikizo na maneno ya chuki kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Azziad kurejea nchini Kenya akitokea Marekani, ambako alikuwa katika ziara ya kikazi. Ziara hiyo ilihusisha shughuli mbalimbali za kazi na kukutana na wadau wa sekta ya ubunifu, jambo ambalo pia limechangia kuibua mjadala mpana kuhusu maendeleo yake ya kimataifa.