Mtayarishaji wa maudhui mtandaoni, Dem Wa Facebook, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea kiti cha Mwakilishi wa Wanawake katika Uchaguzi Mkuu nchini Kenya wa mwaka 2027.
Kupitia ukurasa zake za mitandao ya kijamii, Dem Wa Facebook ameposti bango la kampeni lililoambatana na ujumbe ulioibua mjadala mkubwa mtandaoni, akiwahoji wananchi iwapo mwaka 2027 ni wakati mwafaka kwake kuwania nafasi hiyo au kama anapaswa kusubiri hadi 2032 baada ya kura kuchukuliwa.
Katika tangazo hilo, Dem Wa Facebook ameweka wazi vipaumbele vya manifesto yake ambavyo vinajikita katika uwazi na uwajibikaji, kuinua uchumi wa wanawake, kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo uwakilishi wa haki na sauti halisi katika uongozi.
Hatua hii inamuweka Dem Wa Facebook miongoni mwa wanawake wanaojitokeza kuwania nyadhifa za uongozi kuelekea uchaguzi wa 2027, hali inayodhihirisha mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea nchini Kenya, hususan kuibuka kwa viongozi wapya wanaotumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kufikisha ajenda zao kwa umma.