Msanii mkongwe kutoka Uganda, Bebe Cool, amefichua kuwa serikali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha mfumo wa kutoa leseni kwa watengenezaji wa maudhui ya kidijitali wanaofanya kazi kupitia majukwaa kama YouTube na TikTok.
Akizungumza kwenye moja ya podcast nchini humo, Bebe Cool alisema mpango huo unalenga kudhibiti maudhui ya mitandaoni na kuhakikisha matumizi yenye uwajibikaji wa majukwaa ya kidijitali. Amesema content creators watalazimika kupata leseni rasmi ili kuendelea kufanya shughuli zao kihalali nchini Uganda.
Msanii huyo, ameunga mkono mpango huo akisema utasaidia kupunguza matamshi ya chuki mitandaoni, upotoshaji wa habari na unyanyasaji wa kidijitali.
Bebe Cool anaamini kuwa hatua ya kutoa leseni kwa watengenezaji wa maudhui itahimiza uwajibikaji na nidhamu katika matumizi ya mitandao ya kijamii, huku ikilinda jamii dhidi ya maudhui hatarishi na ya kupotosha.