Msanii wa muziki wa injili nchini Kenya, Jimmy Gait, amenusurika kifo mapema leo baada ya kuvamiwa na kushambuliwa vibaya na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi .
Kwa mujibu wa swahiba wake wa karibu DJ Mo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea leo majira ya saa nne asubuhi katika mtaa wa kifahari wa Runda, Nairobi, ambapo msanii huyo alikumbana na wahuni waliomwachia majeraha mabaya mwilini.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, DJ Mo amesema wahuni hao walifanikiwa kupora simu ya mkononi ya msanii huyo, jambo ambalo limezua hofu ya uwezekano wa kutokea kwa utapeli.
Hata hivyo, ametoa tahadhari kwa umma kuwa waangalifu na mawasiliano yoyote yatakayotoka kwenye namba ya Jimmy Gait kwa sasa, akisema kuwa huenda wahalifu hao wakatumia kuwahadaa Wakenya.