Penzi la bosi wa Konde Music Worldwide, Harmonize, kwa malkia wa filamu Bongo Kajala Masanja, limeingia kwenye hatua nyingine baada ya msanii huyo kutoa viapo vizito vinavyovuka mipaka ya dunia mbele ya mpenzi wake huyo.
Kupitia mfululizo wa video fupi (Instastories) akiwa ndani ya gari na Kajala, Harmonize ameonekana akimwaga maneno ya mahaba yaliyojaa hisia kali, akijinasibu kuwa upendo wake kwa Kajala hauna mbadala, hata huko akhera.
Harmonize amesikika akisema kuwa mapenzi yake ni ya kipekee kiasi kwamba, hata ikitokea amefika mbinguni na kupewa zawadi ya Malaika wa Peponi, atawakataa wote na kuomba apewe mwanamke mmoja tu ambaye ni Kajala.
Hata hivyo, kilichovunja mbavu za wafuasi wao, ni jibu la papo hapo la Kajala Masanja. Badala ya kuyeyushwa na viapo hivyo vya mahaba, amejibu kwa utani wa ucheshi uliotilia shaka ukweli wa maneno ya Harmonize kwa kumuita msanii huyo muongo.
“Rajabu ni muongo jamani… mimi nitakuwa motoni,” amesema Kajala huku akicheka, kauli ambayo imetafsiriwa na wengi kama utani wa mahaba uliolenga kuonyesha jinsi wawili hao walivyo huru kutaniana katika uhusiano wao.