Memba wa kundi la 34 Brick kutoka mtaa wa Eastlands, Mauru Gwaash, amefunguka baada ya kushambuliwa pamoja na wasanii wa kundi hilo rapa Toxic Lyrikali na Oush katika eneo la Kiamaiko, Nairobi.
Kupitia Instastory yake, Mauru amesema kuwa tukio hilo halihusiani kwa namna yoyote na makundi ya muziki ya Buruklyn Boyz wala Wakadinali, licha ya wengi kuhisi kuwa huenda lilikuwa sehemu ya bifu inayoendelea kwenye tasnia ya rap nchini Kenya.
Hata hivyo, msanii huyo ambaye anadaiwa kuwa anauguza majeraha ya uvamizi, ameweka wazi kuwa kilichotokea hakikuwa na uhusiano wowote na mzozo wa kimuziki. Amesema kuwa shambulio hilo lilifanywa na watu anaowafahamu, akiwataja kama marafiki waliokuwa na wivu na masuala binafsi ambayo hayahusiani na muziki.
Shambulio hilo lilitokea Jumapili, siku moja tu baada ya Mauru Gwaash kwenda live Instagram ambapo aliwakosoa vikali makundi ya muziki ya Wakadinali na Buruklyn Boyz. Tukio hilo pia limekuja mara baada ya rapa Toxic Lyrikali kuachia wimbo wake wa diss uitwao “Bad Everyday” uliowalenga wasanii wa Buruklyn Boyz.