
Mtayarishaji maarufu wa filamu, Abel Mutua, ameonekana kushangazwa na tabia ya Wakenya kupendelea kushabikia au kusambaza matukio ya matusi, vurugu, na drama kuliko yale yanayohusisha tabia njema au ujumbe wa heshima.
Kupitia Instagram, Abel ameelezea masikitiko yake jinsi baadhi ya watu maarufu nchini wanavyojulikana si kwa matendo yao mema, bali kwa visa vya vurugu. Ametoa mfano wa mhubiri maarufu Pastor James Ng’ang’a, akisema kuwa video zinazopata umaarufu zaidi kwenye mitandao ya kijamii ni zile zinazomwonyesha akiwatukana, akipiga kelele, au akitishia waumini wake.
Kwa mujibu wa Abel, hali hii inaonyesha taswira ya jamii ambayo imeanza kuona matusi na fujo kama sehemu ya burudani, huku watu wenye ujumbe wa maana na heshima wakipuuzwa au kutopewa nafasi mitandaoni.
Hata hivyo amesema kuwa hali hii si tu inawakatisha tamaa watu wenye maadili mema, bali pia inaathiri kizazi kipya ambacho sasa kinaamini kuwa njia ya kupata umaarufu ni kwa kuwa wa matusi au drama mitandaoni.