Entertainment

Akothee Amwandikia Rais Ruto: “Tufungue Mlango wa Mazungumzo”

Akothee Amwandikia Rais Ruto: “Tufungue Mlango wa Mazungumzo”

Mwanamuziki, mfanyabiashara, na mwanaharakati wa kijamii Akothee maarufu kama Rais wa Akina Mama Wasio na Wenzi, ameandika barua ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, akitoa kilio cha kina kwa niaba ya akina mama, vijana, wazazi, na wajasiriamali nchini.

Katika barua hiyo yenye hisia nzito, Esther anasema haandiki kama mtu maarufu tu, bali kama mzazi anayeishi na vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano ya hivi karibuni kote nchini.

“Nakuandikia si tu kama raia, bali kama mama, mama asiye na mwenzi wa vijana wa Gen Z – na kama Mkenya ambaye bado anaamini katika roho ya taifa hili,” alianza kwa maneno yenye kugusa moyo.

Esther anaelezea hali ya taifa kwa sasa kuwa ya kusikitisha, mitaa imejaa hofu, anga limefungwa na huzuni, na familia pamoja na biashara ziko katika hali ya taharuki. Anasema vijana na wananchi kwa ujumla hawatafuti tu mabadiliko ya sera, bali wanalilia usalama, uthabiti, na uongozi unaosikiliza.

“Wakenya sasa hawapigi kelele kwa mabadiliko tu. Wanapaza sauti kwa ajili ya usalama, uthabiti na uelewa. Wanataka uongozi unaosikiliza; nchi ambayo watoto wao wanaweza kwenda shule bila vurugu, biashara kufunguliwa bila hofu ya uporaji, na familia zisizopoteza wapendwa kwa risasi au kipigo,” alieleza kwa uchungu.

Esther pia anahoji uhalali wa taifa kuhubiri amani ulimwenguni huku picha halisi ya ndani ikionyesha vurugu, mauzoo ya matumaini, na uharibifu wa kiuchumi unaowatesa wananchi wa kawaida.

Akitilia mkazo kuwa barua hiyo si ya lawama, bali ya uwajibikaji wa pamoja, anamtaka Rais kuchukua hatua ya kidiplomasia ya kuanzisha mazungumzo ya kweli.

“Hili si suala la lawama. Ni kuhusu uwajibikaji wa pamoja. Tukivutana, tunapoteza sote. Na anayepoteza zaidi ni Kenya.”

Kama mama, anasema anaelewa kiu ya vijana kusikilizwa, ndiyo maana baadhi yao walijaribu kuingia bungeni. Sio kwa fujo, bali kama njia ya kuonyesha kutotambuliwa kwao katika maamuzi ya taifa.

Alihitimisha barua hiyo kwa ombi la moja kwa moja kwa Rais, kuwakutanisha na wazazi, akina mama, na vijana Ikulu kwa mazungumzo ya wazi.

“Nakuomba kwa unyenyekevu unikubalie nafasi ya kusikilizwa, si kwa ajili yangu tu, bali kwa ajili ya mama wote, wazazi, na vijana wetu. Tufungulie mlango. Tuweke tofauti kando. Tufikirie pamoja. Natumaini mazungumzo yanaweza kuokoa roho ya taifa hili.”

Barua hiyo imeendelea kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengi wameisifu kama sauti ya ujasiri, huruma, na matumaini, sauti inayozungumza kutoka moyoni mwa mzazi wa kawaida hadi juu ya meza ya mamlaka.