
Kampuni ya Google imeongeza kipengele kipya katika toleo jipya la Android 16 kinachoitwa Live Updates, ambacho sasa kinapatikana kwenye sehemu ya Notifications na Lock Screen za simu.
Mfumo huu mpya wa Live Updates umeundwa kusaidia watumiaji kufuatilia taarifa zinazoendelea kubadilika kwa wakati halisi, kama vile matokeo ya mechi za moja kwa moja, hali ya trafiki, ratiba za usafiri wa umma, au huduma za usafirishaji kama vile magari ya ride-hailing. Taarifa hizi sasa zinaweza kuonekana moja kwa moja kwenye skrini ya simu hata bila kuifungua.
Kwa mfano, mtumiaji anaweza kuona mabadiliko ya moja kwa moja ya alama za mechi au mahali gari lake lilipo bila kulazimika kufungua programu husika. Hii inaleta urahisi mkubwa hasa kwa wale wanaotegemea taarifa za papo kwa hapo katika shughuli zao za kila siku.
Google imesema kuwa Live Updates zitafanya kazi kwa kushirikiana na apps mbalimbali zitakazosasishwa kuunga mkono teknolojia hiyo, huku usalama na faragha za watumiaji zikizingatiwa.
Kipengele hiki kinatarajiwa kuwavutia sana watumiaji wa Android waliokuwa wakitamani urahisi zaidi katika upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati unaofaa. Toleo kamili la Android 16 linatarajiwa kusambazwa kwa simu mbalimbali kuanzia mwisho wa mwaka huu.