
Digital creator maarufu nchini Kenya, Baba Talisha, ameweka wazi kwa mara ya kwanza sababu inayomfanya bado hajamuoa rasmi mchumba wake, Miss Wanjey, licha ya uhusiano wao kudumu kwa muda na kuvuma mitandaoni.
Katika mahojiano yake hivi karibuni, Babatalisha alifunguka kuhusu kiapo alichompa mke wake wa zamani kabla ya kifo chake, ahadi ya kumalizia mahari aliyokuwa ameanza kulipa kwa familia ya marehemu. Kwa mujibu wa Babatalisha, dhamira hii ni ya moyoni na anahisi lazima aitimize kikamilifu kabla hajaanza safari mpya ya ndoa.
“Nilimwahidi marehemu mke wangu kwamba nitatimiza kila kitu nilichoanzisha kama mume wake. Hiyo ni heshima ninayomdhaminia hadi leo,” alisema Babatalisha kwa sauti ya kutetemeka.
Ingawa mashabiki wengi wamekuwa wakimtaka kuoa rasmi Miss Wanjey, ambaye pia ni maarufu kwa maudhui ya mtandaoni na mpenzi wake wa sasa, Babatalisha anasema hana haraka, kwani anataka kila hatua ya maisha yake ya ndoa ijengwe kwa misingi ya heshima na ukamilifu wa moyo.
“Siwezi kufungua ukurasa mpya bila kufunga wa zamani kwa heshima na utimilifu,” aliongeza.
Mashabiki wameonyesha kuelewa msimamo wake huku wengi wakimsifu kwa kuwa na maadili ya kipekee na kuonyesha mfano wa kuheshimu ndoa hata baada ya kifo.
Uhusiano wa Babatalisha na Miss Wanjey umekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii kutokana na vichekesho vyao vya mapenzi, changamoto za kila siku, na uhalisia wa maisha yao ya pamoja. Hata hivyo, sasa mashabiki wana mtazamo mpya kuhusu uzito wa maamuzi anayopitia Babatalisha.