Entertainment

Bebe Cool Aeleza Sababu ya Wasanii wa Afrika Mashariki Kusalia Nyuma Kisanaa

Bebe Cool Aeleza Sababu ya Wasanii wa Afrika Mashariki Kusalia Nyuma Kisanaa

Mwanamuziki mkongwe kutoka Uganda, Bebe Cool, ameonyesha masikitiko yake kuhusu hali ya muziki wa Afrika Mashariki, akieleza kuwa miaka 15 iliyopita wasanii wa ukanda huo walikuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kimataifa lakini walikosa kuendeleza juhudi hizo.

Kwa mujibu wa Bebe Cool, kipindi hicho kulikuwa na umaarufu mkubwa ambao ulipaswa kutumiwa kama daraja la kuingia katika soko la kimataifa. Hata hivyo, anasema wasanii wengi waliridhika mapema na kupoteza ari ya kusonga mbele.

Ametoa mfano wa wasanii kutoka Nigeria ambao waliendelea kusukuma juhudi zao na sasa wamefanikiwa kutamba duniani, huku wenzao wa Afrika Mashariki wakibaki nyuma.

“Miaka 15 iliyopita tulikuwa juu sana, lakini hatukuitumia nafasi hiyo vizuri. Wasanii wa Afrika Mashariki tuliridhika, tukakata tamaa, huku wenzao wa Nigeria wakiendelea kusonga mbele,”  Alisema akizungumza na runinga ya K24.

Kauli yake imeibua mijadala mitandaoni, wengi wakimtaka kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kushirikiana na wasanii wachanga ili kufufua na kuimarisha muziki wa Afrika Mashariki. Lakini pia wametoa wito kwa wasanii wa ukanda huo kurejea katika ushindani wa kimataifa kwa kujifunza kutoka kwa mafanikio ya wasanii wa Nigeria kama Burna Boy, Wizkid, na Davido.

Bebe Cool anahesabiwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa muziki wa kizazi kipya katika ukanda huu, akiwa na mchango mkubwa katika kukuza dancehall na reggae.