
Msanii nguli wa Afro-pop kutoka Kenya, Bien-Aimé Baraza, ameonekana akiendelea kupanda ngazi za kimataifa baada ya kukutana na msanii mashuhuri wa Nigeria, Burna Boy, katika studio za BBC Radio 1 mjini London. Mkutano huo, ambao umevutia maelfu ya mashabiki mtandaoni, unazua tetesi za uwezekano wa ushirikiano wa kisanii kati ya wawili hao.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bien alipakia video akiwa kwenye studio pamoja na mchekeshaji wa Kimataifa, Edie Kadi, huku akidokeza ujio wa wimbo mpya.
“Onwards and upwards! Had a good time with @comediekadi at @bbcradio1. New single loading… stay tuned. 🔥🎶 Get your tickets for Hamburg, O2, and Kenya tour. Link in bio! Don’t suffer like your enemies,” Bien aliandika kwenye Instagram yake baada ya mkutano huo.
Kauli hiyo imeibua msisimko mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa mkutano wake na Burna Boy umetokea muda mfupi kabla ya ujumbe huo. Ingawa Bien hakutaja moja kwa moja kuhusu ushirikiano na Burna Boy, mashabiki wameanza kuunganisha nukta na kutarajia collabo ya kimataifa inayoweza kutikisa muziki wa Afrika.
Bien, ambaye kwa sasa anazunguka Ulaya kwa ajili ya ziara na mahojiano, ameendelea kujijenga kama msanii wa kujitegemea tangu kundi la Sauti Sol lipumzike kwa muda. Kwa upande mwingine, Burna Boy anaendelea kutamba duniani na amekuwa mstari wa mbele kuipeperusha bendera ya Afrobeats kwenye majukwaa ya kimataifa.