Gossip

Cardi B Aibua Sintofahamu Baada ya Kufuta Picha za Stefon Diggs

Cardi B Aibua Sintofahamu Baada ya Kufuta Picha za Stefon Diggs

Mashabiki wa rapa maarufu Cardi B wameibua hisia mseto mitandaoni baada ya kugundua kuwa msanii huyo amefuta picha zote za mpenzi wake mpya, Stefon Diggs, kutoka kwenye ukurasa wake wa Instagram. Hatua hiyo imezua tetesi kuwa huenda uhusiano wao umeingia matatizoni au hata kuvunjika kabisa.

Wengi wa mashabiki walieleza mshangao na masikitiko, wakikumbuka jinsi penzi la Cardi na Stefon lilivyokuwa linaonekana kuwa la kipekee, lenye mapenzi ya dhati na hadhi ya juu. Wengine walitafsiri hatua hiyo kama njia ya Cardi kujilinda dhidi ya maisha ya umma, huku baadhi wakiamini ni dalili ya mgogoro wa kimapenzi unaoendelea kisiri.

Penzi kati ya Cardi B na Stefon Diggs lilianza rasmi mwezi Juni 2025, walipoonekana kwa mara ya kwanza hadharani wakiwa kwenye boti ya kifahari, wakifurahia muda wao pamoja. Baadaye walihudhuria kwa pamoja Paris Fashion Week na mechi ya mpira wa vikapu jijini New York kati ya Knicks na Celtics, hali iliyothibitisha wazi kuwa walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Katika tamasha la Cannes, Cardi alionyesha upendo wake kwa Stefon kwa kuchora jina lake kwenye kucha zake, jambo lililozua gumzo mitandaoni. Mwisho wa mwezi Juni, wawili hao walikwenda mapumzikoni nchini Ufaransa ambapo Stefon alimkodishia Cardi kasri la kifahari kwa ajili ya likizo ya faragha.

Hata hivyo, kufutwa kwa picha hizo kumezua hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa uhusiano huo, hasa ikizingatiwa kuwa Cardi bado yuko katika mchakato wa talaka kutoka kwa mume wake wa zamani, Offset.

Mashabiki sasa wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kutoka kwa mmoja wao ili kufahamu hatima ya penzi hili lililoanza kwa kishindo.