
Casandra “Cassie” Ventura, mpenzi wa zamani wa rapa maarufu Sean “Diddy” Combs, amewasilisha ombi rasmi mahakamani akiomba msanii huyo asiachiliwe kwa dhamana, akieleza kuwa usalama wake uko mashakani endapo ataachiliwa kabla ya hukumu kutolewa.
Katika barua iliyowasilishwa kwa Jaji Arun Subramanian, Cassie amesema anahofia maisha yake na usalama wa mashahidi wengine waliohusika katika kesi hiyo. Anadai kuwa Diddy ana uwezo mkubwa wa kushawishi, kutisha, au kuzuia ushahidi kutoka kwa mashahidi muhimu ikiwa atakuwa huru nje ya gereza.
Kesi dhidi ya Diddy imekuwa gumzo kubwa nchini Marekani, ikihusisha madai mazito ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono. Ingawa alisafishwa kwenye mashtaka makubwa ya usafirishaji wa binadamu na uhalifu wa mtandao (racketeering), bado alipatikana na hatia ya makosa mawili madogo yanayohusiana na usafirishaji kwa nia ya kufanya ukahaba.
Cassie, ambaye alikuwa mmoja wa mashahidi muhimu, alitoa ushuhuda wa kina mahakamani, akieleza jinsi alivyoathirika wakati wa uhusiano wake na Diddy. Ushuhuda wake uliungwa mkono na mashahidi wengine ambao pia wamewasilisha barua za kuomba Diddy asipewe dhamana hadi kesi hiyo itakapokamilika.
Mawakili wa serikali wamesisitiza kuwa Diddy ni mtu mwenye ushawishi mkubwa na mali nyingi, hivyo anaweza kutumia nafasi ya dhamana kuharibu ushahidi au kutoroka. Wamependekeza adhabu ya kifungo cha kati ya miaka minne hadi mitano kwa makosa aliyopatikana nayo.
Kwa upande wa utetezi, mawakili wa Diddy wameomba apewe dhamana ya dola milioni moja, huku wakiahidi kuwa atakabidhi pasipoti yake na kuwekwa chini ya uangalizi wa kifaa cha kielektroniki (GPS). Wanasema Diddy hajawahi kukiuka masharti ya mahakama tangu mashitaka yaanze na kwamba ana familia na biashara zinazomfungamanisha na Marekani.
Jaji Subramanian bado hajatoa uamuzi kuhusu ombi hilo la dhamana. Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa ndani ya siku chache zijazo, na utakuwa muhimu katika kuamua ikiwa Diddy atasubiri hukumu yake akiwa nje au ataendelea kuzuiliwa gerezani.