Sports news

Crystal Palace Yaandika Historia kwa Kuitandika Manchester City na Kutwaa Kombe la FA

Crystal Palace Yaandika Historia kwa Kuitandika Manchester City na Kutwaa Kombe la FA

Katika moja ya matukio ya kushangaza zaidi kwenye historia ya soka ya Uingereza, Crystal Palace waliibuka mabingwa wa Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe zaidi ya miaka 120 iliyopita, baada ya kuichapa Manchester City bao 1-0 katika Uwanja wa Wembley mbele ya maelfu ya mashabiki.

Mchezo huo uligubikwa na kasi, presha na kiwango cha hali ya juu, lakini lilikuwa ni goli la mapema la Eberechi Eze katika dakika ya 16 lililoamua hatima ya mechi. Eze alimalizia kwa ustadi mkubwa pasi ya chini kutoka kwa Daniel Muñoz, baada ya kushirikiana kwa kasi na Mateta katika mfululizo wa pasi safi kwenye eneo la hatari la City.

Licha ya City kumiliki mpira kwa zaidi ya asilimia sabini na saba, hawakuweza kuvunja ukuta imara wa Palace, huku kipa Dean Henderson akicheza kwa kiwango cha juu na kuokoa mashambulizi kadhaa hatari  ikiwemo penalti ya Omar Marmoush na shuti kali la Jeremy Doku.

Kocha wa Palace, Oliver Glasner, ambaye alichukua timu katikati ya msimu, sasa ameweka jina lake kwenye vitabu vya historia kwa kuwa kocha wa kwanza kutoka Austria kutwaa Kombe la FA. Akizungumza baada ya mchezo, Glasner alisema:

 “Tulihitaji kuwa wakamilifu leo, na kwa kweli wachezaji walionyesha umoja, nidhamu na moyo mkubwa. Huu ni ushindi wa kila mmoja wetu.”

Kwa Manchester City ya Pep Guardiola, kipigo hicho kimehitimisha msimu bila kutwaa taji lolote jambo ambalo halijawahi kutokea tangu msimu wa 2016/17. Licha ya kufanya mashambulizi 23, ukosefu wa ufanisi na umakini katika nafasi muhimu uliwagharimu.

Guardiola alikiri kuwa walikosa makali:

“Tulimiliki mpira, lakini hatukufanya maamuzi mazuri katika eneo la mwisho. Palace walijipanga vyema, hongera kwao.”

Kwa ushindi huu, Crystal Palace wamejihakikishia tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Ligi ya Europa msimu ujao hatua kubwa kwa klabu ambayo wengi walidharau uwezo wake msimu huu. Mashabiki waliokuwa Wembley walisherehekea kwa hamasa kubwa, huku wakishuhudia timu yao ikiandika historia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *