Entertainment

Daddy Owen Aguswa na Video ya Raila Akiimba Jamaica Farewell

Daddy Owen Aguswa na Video ya Raila Akiimba Jamaica Farewell

Msanii wa nyimbo za injili, Daddy Owen, amefunguka namna kifo cha Raila Amollo Odinga kilivyomgusa baada ya kuona video inayomuonyesha kiongozi huyo akiimba wimbo wa “Jamaica Farewell” wa Harry Belafonte.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Daddy Owen amesema alipoamka asubuhi na kukutana na video hiyo, alihisi kuguswa kwa kina na mara moja akaingia YouTube kusikiliza wimbo huo mzima. Amesema alipofika kwenye sehemu ya maoni, aligundua kuwa karibu asilimia tisini ya maoni yalikuwa kutoka kwa Wakenya waliokuwa wakitoa heshima zao kwa Raila.

Msanii huyo amesema tukio hilo lilimfanya kutafakari jinsi muziki unavyounganisha watu na kuvuka vizazi. Ameeleza kuwa ingawa wimbo huo ni wa miaka mingi iliyopita, umepata umaarufu upya miongoni mwa Wakenya kutokana na mapenzi ya Raila kwa muziki.

Daddy Owen ametumia tukio hilo kutoa wito kwa wasanii chipukizi kutokata tamaa katika safari yao ya muziki, akisema muziki ni chombo chenye nguvu ya kuleta mabadiliko na kuishi hata baada ya msanii kuondoka duniani.

Hata hivyo amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba Raila ataendelea kukumbukwa kama kiongozi aliyethamini sanaa na aliyetumia maisha yake kuleta matumaini na mshikamano miongoni mwa watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *