
Msanii wa Injili nchini Kenya, Daddy Owen, ameibua mjadala mkubwa mtandaoni baada ya kutoa ushauri kwa wanaume kuhusu ndoa, akisisitiza kuwa msingi wa ndoa haupaswi kuwa mapenzi pekee, bali kuelewa kusudi la maisha.
Kupitia chapisho lake la Instagram, msanii huyo alisema:
“Kama mwanaume, usioe kwa sababu ya mapenzi. Oa kwa sababu ya kusudi. Nilifikiri ndoa ni kuhusu mapenzi, kumbe sio.”
Msanii huyo alifafanua kauli yake kwa kusema kuwa wanaume wengi huingia kwenye ndoa wakiwa hawajajitambua wala kuelewa malengo yao ya maisha, hali inayochangia migogoro na kuvunjika kwa ndoa.
“Kama kusudi lako halijajulikana, hiyo ni kama mabomu yanayosubiri kulipuka. Wanaume huoa chini ya kiwango chao kwa sababu hawajajua walipoelekea. Ukijua kusudi lako, mwanamke atajivuta kwenye hilo kusudi,” aliongeza.
Kauli hii imepokewa kwa hisia tofauti kutoka kwa mashabiki wake, baadhi wakimsifu kwa mtazamo wa kiroho na msingi wa maisha yenye maono, huku wengine wakitofautiana naye, wakisema mapenzi bado yana nafasi kubwa katika ndoa yenye mafanikio.
Daddy Owen, ambaye amepitia changamoto katika maisha yake ya ndoa hapo awali, anaonekana kutumia uzoefu wake kuwashauri vijana wanaopanga kuoa, akisisitiza umuhimu wa kujitambua kabla ya kuingia katika hatua hiyo muhimu ya maisha.
Ujumbe wake umeendelea kuvutia mijadala kuhusu maana ya ndoa katika kizazi cha sasa, na umuhimu wa kuwa na msingi imara wa maisha kabla ya kuchukua jukumu la kifamilia.