
Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, ameonesha kutoridhishwa na hatua ya jina na picha yake kutumiwa na ukurasa maarufu wa mitandaoni nchini kwao, katika mjadala kuhusu kwa nini wasanii wa Tanzania hushindwa kusainiwa na lebo kubwa za kimataifa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond amejibu vikali mada hiyo, akieleza kuwa amekuwa na mafanikio makubwa katika anga za kimataifa. Amesema amewahi kupokea ofa kutoka kwa lebo kubwa duniani kama Universal Music Group na Roc Nation, na hatimaye alisaini mkataba rasmi na Warner Music, unaokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi bilioni 13.5 za Kitanzania.
Msanii huyo ambaye pia ni mkurugenzi wa lebo ya WCB Wasafi, amesema mafanikio yake hayakuja kwa bahati bali ni matokeo ya bidii, maadili ya kazi na kujituma kwake. Ametaja kuwa amewahi kushirikiana na mastaa wa kimataifa kama Alicia Keys, Rick Ross, Ne-Yo, Omarion na wengine wengi, ishara kuwa anaheshimiwa na kutambuliwa hata nje ya mipaka ya Afrika.
Kauli hiyo imeibua mjadala mpana mitandaoni, huku mashabiki wake wakimtetea vikali, wakisisitiza kuwa Diamond ni miongoni mwa wasanii wachache barani Afrika walioweza kuvuka mipaka ya bara na kupata nafasi katika jukwaa la kimataifa.