
Mwanamitandao aliyegeukia muziki Diana Marua amefuta video aliyotengeneza akidai kuwa staa wa muziki nchini Willy Paul alijaribu kumbaka.
Hii ni baada ya mahakama ya Milimani kutoa amri ikimtaka Diana Marua kufuta video ambayo alipakia YouTube mnamo Desemba 9 yenye jina la ‘My Untold Story, Willy Paul tried to rape me’ ikielezwa kuwa madai yake yameathiri kazi na afya ya Willy Paul .
“Inaamriwa kuwa video ya mshtakiwa/mlalamikiwa na chapisho la mitandao ya kijamii lililochapishwa kwenye chaneli yake ya YouTube yenye jina la ‘My Untold Story, Willy Paul tried to rape me’, lfutwe ikusubiriwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi yake kwa vile linamuathiri mlalamishi, kumfanya apoteze fursa za biashara na kumfanya ateseke kiafya” Karatasi ya amri za mahakama iliyotiwa saini na hakimu mkuu mwandamizi D.W Mburu ilisomeka.
Mahakama pia ilimtahadharisha Diana na washirika wake dhidi ya kumharibia jina Willy Paul ikisubiriwa kusikilizwa kwa kesi aliyowasilisha mahakamani. Onyo kali imetolewa kwa yeyote atakayekaidi amri hiyo ya mahakama ambayo ilitolewa tarehe 29 Desemba.